Usajili wa beki Kelvin Yondani ndani ya kikosi cha Polisi Tanzania FC, umempa jeuri kocha mkuu wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa pili mfululizo.
Kocha Malale Hamsini amesema beki huyo atakua msaada mkubwa kikosini kwake, kutokana na kuwa na uzoefu wa kutosha katika ushindani wa Ligi Kuu, hivyo hana saka la safu yake ya ulinzi ambayo itakua na mkongwe huyo.
Amesema kwa kipindi cha miezi kadhaa kikosi chake kilikua kinakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na safu nzuri ya ulinzi, na kujikuta wakiruhusu mabao mepesi dhidi ya timu pinzani za Ligi Kuu, hivyo ujio wa beki huyo wa zamani wa klabu za Simba SC na Young Africans utamsaidia kwa kiasi kikubwa.
“Kuwa na mchezaji mzoefu kama Yondani kwenye kikosi ni jambo zuri kwani ni mchezaji ambaye amecheza kwa kiwango cha juu kwenye timu kubwa, hivyo uzoefu wake utakuwa msaada mkubwa kwetu kutokana na kikosi chetu kuwa na idadi kubwa ya vijana.”
“Tulikuwa na tatizo kwenye safu yetu ya ulinzi jambo ambalo lilipelekea tuwe tunaruhusu mabao mepesi kwenye mechi zetu, hivyo uwepo wa Yondani kikosini kwa kiasi kikubwa utaongeza umakini kweye safu ya ulinzi kutokana na uzoefu alionao.” Amesema kocha Malale
Yondani aliesajiliwa na maafande hao katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, alicheza mchezo wake wa kwanza akiwa na Polisi Tanzania juzi Jumanne (Januari 05) kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Ndanda FC, waliokubali kufungwa bao moja kwa sifuri.