Saa chache baada ya Bodi ya Ligi Tanzania, (TPLB) kuthibitisha mabadiliko ya tarehe ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Young Africans dhidi ya Simba SC, pande hizo mbili zimetoa kauli juu ya mbadiliko hayo.
Mapema hii leo TPLB walitoa taarifa ya mabadiliko ya ratiba ya mchezo huo ambao ulipangwa kupigwa Oktoba 18, na sasa umesogezwa mbele hadi Novemba 07, huku uwanja ukibaki kuwa Benjamin Mkapa Dar es salaam.
Taarifa imefafanua kwamba kwa sasa nchi nyingi bado zinaendelea kuwa na vikwazo vingi kwenye masuala ya usafiri kutokana na janga la Virusi vya Corona kuendelea kusumbua nchi nyingi, hivyo kuna wasiwasi baadhi ya wachezaji walioitwa kwenye timu zao za taifa wakashindwa kuwasili nchini kwa wakati.
Afisa Mhamasishaji wa Young Africans, Antonio Nugaz amesema wamefurahishwa na mabadiliko hayo, kwani wanaamini itawapa nafasi ya kukiandaa vyema kikosi chao kuelekea Novemba 07.
Nugaz amesema kwa muda walioupata, kikosi chao kitakua chini ya kocha wanaetarajia kumtangaza, na wanaamini kocha huyo atafanya kazi yake ipasavyo ili kufanikisha ushindi kwenye pambano hilo ambalo linasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.
“Ni faraja kwetu, maana kikosi kitapata nafasi ya kujiandaa vizuri, kocha tunaetarajia kumtangaza atapata wasaa wa kukaa na wachezaji wake, na kutengeneza mbinu zitakazotupa furaha siku hiyo ya Novemba 07.” Amesema Nugaz.
Kwa upande wa Simba SC, nao wamekiri kuipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili, huku wakiamini tarehe ya mabadiliko iliyotajwa na TPLB itatoa wasaa mzuri kwa kikosi chao kujenga umakini mkubwa.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema wamepokea taarifa hizo za mabadiliko ya ratiba, na wameshaanza kuzifanyia kazi.
“Tumepokea taarifa kupelekwa mbele kwa mchezo wetu na tutazifanyia kazi kwa ukaribu ndani ya Simba,” amesema.
Kabla ya mchezo huo, Simba na Young Africans zilikuwa zimecheza michezo mitano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku zote zikimiliki alama 13.
Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu na Young Africans inashika nafasi ya tatu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.