Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kimeendelea na Mazoezi ya Gym kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Mzunguuko wa Tatu wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC utakayopigwa Septemba 6, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Meneja wa klabu hiyo, Walter Harrison, amesema kuwa wachezaji wote wa timu hiyo, kasoro wale waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ wamerejea kambini, huku wachezaji walioumia kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union, Yannick Bangala na Jesus Moloko wakiendelea vizuri.
“Tuko kwenye mazoezi ya utimamu wa mwili ‘Gym’ ambayo ndiyo tumeanza nayo, kikosi kizima kiko mazoezini kasoro wale tu ambao walikuwa kwenye timu ya taifa. Lengo ni kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu inayokuja dhidi ya Azam FC, lakini siku chache tu baada ya hapo tutakuwa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati yetu na Zolan FC,” amesema Harrison.
Kuhusu Zolan FC, kuomba kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kama Uwanja wao wa nyumbani, Harrison amesema hilo lilikuwapo, lakini litatolewa taarifa baadaye kwani linaratibiwa kwa pamoja kati ya viongozi wa klabu yake na wale wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’.
“Na suala la mchezo ya kirafiki ni mpaka tuwasiliane na Kocha Nabi atuambie ni aina gani ya timu ambayo anaihitaji, kwa kweli kwa muda uliopo ni lazima kupata mchezo wa kirafiki. Kingine ni kwamba majeruhi wetu wanaendelea vizuri, kama utakumbuka tulizalisha majeruhi wawili kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union, Jesus Moloko na Yannick Bangala.
Young Africans itacheza mchezo wa kwanza nyumbani msimu huu dhidi ya Azam FC, baada ya kuanza msimu ikiwa ugenini Jijini Arusha kwa kucheza dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union.