Kikosi cha Singida Big Stars kitaweka Kambi jijini Mwanza kujiandaa na mchezo wa Mzunguuko wa Tatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Singida Big Stars iliyoanza msimu wa 2022/23 kwa kucheza nyumbani Uwanja wa Liti mjini Singida dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City, itacheza Ugenini kwa mara ya kwanza dhidi ya Dodoma Jiji Septemba 06.

Msemaji wa Klabu hiyo Hussein Massanza amesema mchezo huo wa ugenini utachezwa katika Uwanja wa Liti mjini Singida, kufuatia Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kufungiwa kwa kukosa sifa.

Massanza amesema wanaamini Kambi ya Mwanza itakisaidia kikosi chao kuongeza makali, baada ya kuanza vizuri kwa kukusanya alama sita kwa kuzifunga timu za Mbeya (Mbeya City na Tanzania Prisons).

Amesema wanashukuru kupata matokeo hayo mazuri, lakini hayatoshi kwa sababu wamejiwekea malengo makubwa katika msimu huu wa kwanza, hivyo wamedhamiria kuendelea kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa tatu dhidi ya Dododma Jiji FC.

Kuhusu hali za wachezaji Abdul-Majid Mangalo na Shafiq Batambuze ambao waliumia katika michezo iliyopita, Massanza amesema wawili hao wanaendelea vizuri na tayari wameshaanza mazoezi mepesi.

Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaonyesha Singida Big Stars inashika nafasi ya tatu, ikitanguliwa na Mabingwa watetezi Young Africans na Simba SC iliyo kileleni.

Timu hizo zote zinamiliki alama sita baada ya kushinda michezo miwili ya awali, lakini zimetofautriana mabao ya kufungana kufungwa.

Masoud Djuma aomba radhi Dodoma Jiji FC
Azam FC kulipa kisasi kwa WANANCHI