Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans huenda wakaanza kutetea taji lao msimu ujao 2022/23 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kufuatia Uwanja wa Ushirika Moshi kufungiwa na Shirikisho la Soka ‘TFF’.
Young Africans imepangwa kuanza kutetea Taji la Ligi Kuu kwa kucheza dhidi ya Polisi Tanzania, ambao huutumia Uwanja huo kama Uwanja wake wa nyumbani tangu ilipopanda Ligi Kuu misimu mitatu iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF muda mchache uliopita imeonyesha kuwa, Uwanja wa Ushirika Moshi ni miongoni mwa Viwanja vilivyofungiwa kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu, kufuatia kukosa sifa.
Polisi Tanzania imekua ikiutumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kama Uwanja mbadala, hivyo huenda wakauchagua Uwanja huo kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Young Africans.
Viwanja vingine vilivyofungiwa ni Mabatini-Mlandizi, Pwania (Ruvu Shooting), Mkwakwani-Tanga (Coastal Union), Nyankumbu Girls-Geita (Geita Gold FC) na Jamhuri-Dodoma (Dodoma Jiji FC).
Viwanja vilivyopitishwa kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu msimu ujao 2022/23 ni Benjamin Mkapa (Dar es salaam), Azam Complex (Dar es salaam), Kaitaba (Kagera), Sokoine (Mbeya), Kirumba (Mwanza), Highland Estate (Mbarali-Mbeya), Karatu (Arusha), Liti (Singida), Manungu Complex (Tuariani-Morogoro), Sheikh Amri Abeid (Arusha) na Uhuru (Dar es salaam).