Baada ya kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho la soka nchini TFF, kutangaza hukumu ya sakata la kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison jana Agosti 12, uongozi wa klabu ya Young Africans umeibuka na kusema haujaridhishwa na maamuzi hayo na watahakikisha wanakata rufaa.
Mwenyekiti wa kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, Elias Mwanjala alitangaza hukumu hiyo mbele ya waandishi wa habari baada ya sakata hilo kuchukua siku tatu kusikilizwa kwa kuhusisha pande zote mbili.
Uongozi wa Young Africans kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii umetoa taarifa kuwa haujaridhishwa na uamuzi huo na watakata rufaa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo duniani (CAS).
Young Africans wamesema wanasubiri nakala ya hukumu kutoka kamati husika ili waanze kuchukua hatua.
“Uongozi unawataka wanachama na wapenzi wate kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya klabu yetu”
“Aidha uongozi utaendelea kushirikiana na wadhamini wetu katika kujenga klabu yetu.” imesomeka taarifa hiyo.
Katika maamuzi yaliyotolewa na TFF jana Agosti 12, ni kuwa mchezaji huyo yupo huru na atachagua timu ya kucheza baada ya mkataba wake na Young Africans kuwa na mapungufu.
“Kikao kilikuwa kirefu mpaka kufikia maamuzi haya, malalamiko ya Morrison yalikuwa kwamba hakuongeza mkataba na Yanga, tumeangalia mkataba wake tumeona una mapungufu,” alisema Mwanjala
Hata hivyo, Morrison atapelekwa kwenye kamati ya maadili ya shirikisho la soka nchini TFF, baada ya kusaini mkataba na klabu ya Simba Agosti 8, 2020.
Wakati Young Africans wakitarajia kukata rufaa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo duniani (CAS), Kiungo mshambuliaji wa Alliance, David Richard amedai ana uwezo wa kuziba pengo la Bernard Morrison, huku akihusishwa kuwa mbioni kusajiliwa na klabu hiyo kongwe nchini katika kipindi hiki cha dirisha la usajili kuelekea msimu wa 2020/21.
Msimu uliopita Richard alifunga mabao manane huku akiwa mmoja wa wachezaji waliofunga Hat trik kwenye ya Ligi Kuu Ya Soka Tanzania Bara.
Anasifika kwa kasi na uwezo wake wa kufunga mabao na kushambulia pia kupiga mipira ya faulo ambayo mara nyingi alikuwa mpigaji kwenye kikosi cha Alliance FC, ambacho msimu ujao kitashiriki ligi daraja la kwanza.
Richard amesema yeye anaamini kiwango chake, hivyo yuko tayari kukipiga Yanga au timu yoyote itakayotaka kumsajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.
Amesema kwa sasa yuko jijini Mwanza na tayari ameshapata ofa nyingi lakini kwake anaangalia timu itakayoweza kumlipa masilahi zaidi ndio maana hajasaini mkataba wowote mpaka sasa.
“Mimi Yanga, Simba au klabu yoyote naweza kucheza pasipo kuhofia namba tena nina imani nikicheza hizi timu nitakuwa bora zaidi kwani ndoto yangu ni kuja kuchezea hizi klabu,” amesema Richard.
Hata hivyo, Winga huyo amesema kwake msimu uliopita ulikuwa wa mafanikio makubwa kwani aliweza kucheza michezo 30 ya Ligi Kuu na alikuwa akicheza kwa mara ya kwanza.