Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wanatajwa kukamilisha usajili wa Mshambuliaji wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Ranga Chivaviro pamoja na Kiungo Mshambuliaji kutoka TP Mazembe ya DR Congo Phillipe Kinzumbi.
Young Africans imekuja na mpango mkakati wa kusajili wachezaji wenye uwezo na uzoefu wa michuano ya kimataifa ambao wamezifikisha timu zao kuanzia hatua ya makundi kunako michuano ya Afrika msimu wa 2022/23.
Mmoja wa mabosi wa Young Africans, amesema kuwa mara baada ya Mkutano Mkuu wa Klabu hiyo utakaofanyika Juni 25, mwaka huu, Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Mzambia, Andre Ntine ataanza kukamilisha madili hayo.
Bosi huyo amesema Ntine ataanzia Afrika Kusini kwenda kukamilisha usajili wa Chivaviro ambaye wamefikia makubaliano mazuri ya kusaini mkataba wa awali baada ya kukataa ofa kadhaa ikiwemo ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Ameongeza kuwa, baada ya kukamilisha dili la Chivaviro, siku inayofuatia atasafiri kuelekea DR Congo kwenda kumalizana na Kinzumbi ambaye naye, alishasaini mkataba wa awali.
“Juni 25, mwaka huu mara baada ya Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Young Africans, Ntine ataondoka nchini Tanzania kwenda Afrika Kusini kumalizia makubalino ya mwisho na menejimenti ya mshambuliaji Chivaviro.
“Chivaviro yeye mwenyewe ameonesha nia ya kuja kuichezea Young Africans, hii ni baada ya kukataa ofa ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambao wameonesha nia ya kumsajili lakini mchezaji huyo amegomea ofa yao alitaka kucheza nje ya Afrika Kusini msimu ujao.
“Baada ya hapo Ntine atakwenda DR Congo kwa ajili ya kwenda kukamilisha dili linguine la Kinzumbi ambaye ni chaguo la kocha Nabi ambaye anakuja kuiboresha safu ya ushambuliaji,” amesema Bosi huyo.