Uongozi wa Mabingwa wa Tanzania Bara Young Africans umewashukuru Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kwa ushirikiano waliouonesha Kabla, Wakati na Baada ya mchezo wa Mzunguuko wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Young Africans iliikaribisha TP Mazembe ya DR Congo, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam jana Jumapili (Februari 19) na kupata ushindi wa 3-1.
Shukran kwa Wanachama na Mashabiki wa Young Africans zimetolewa na Uongozi wa Klabu hiyo kupitia kurasa za Kijamii za Klabu hiyo, huku ukiwasisitiza kuendelea kuwa bega kwa bega na timu yao katika kipindi hiki cha kusaka nafasi ya kufuzu Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Taarifa ya Uongozi wa Young Africans iliyochapishwa kwenye Kurasa za Mitandao ya Kijamii: “Shukrani kwa Wanachama, Mashabiki na Wapenzi wa Young Africans SC kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wetu wa kimataifa dhidi ya TP Mazembe kwenye Dimba la Benjamin Mkapa jana.
Hakika ushindi wa jana ni Heshima kwetu, Klabu yetu na Taifa kwa ujumla.”
Young Africans itacheza mchezo wa Mzunguuko wa Tatu wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika Jumapili (Februari 26) dhidi ya Real Bamako ya Mali.
Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam kuelekea Bamako-Mali, baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC utakaopigwa keshokutwa Jumatano (Februari 22).