Klabu ya Young Africans imethibitisha kutuma ofa ya kumsajili beki wa kati wa Coastal Union Bakari Nondo Mwamnyeto, ili kukamilisha mpango wa kumuhamishia mchezaji huyo Jangwani kwa msimu ujao.
Young Africans imetajwa kwa muda mrefu kuwa kwenye mipango ya usajili wa mchezaji huyo, ambaye pia anawania na klabu nyingine kama Simba SC na Azam FC.
Taarifa za kutumwa kwa ofa hiyo zimetolewa na mjumbe wa Kamati ya usajili lakini pia mjumbe wa Kamati ya mabadiliko Young Africans Injinia Hersi Said, ambaye amedhamiria kuiona klabu hiyo ikiwa na kikosi chenye mashiko kuanzia msimu ujao.
Hersi amesema Mwamnyeto bado yupo kwenye rada za Young Africans, na wanaheshimu mkataba uliopo kati yake na Coastal Union, hivyo wamefata njia sahihi kwa kutuma ofa ya usajili.
“Bakari Mwamnyeto ni mchezaji halali wa Coastal Union na ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu.”
“Ni kweli klabu yetu iliona umuhimu wa huduma zake. Tumeshatuma ofa yetu rasmi kwa Coastal kuhusu huduma zake”
“Coastal wao pia wameelezea matakwa yao katika mkataba huo. Sitoweza kutaja mahitaji ya Coastal lakini tumefikia pazuri”
“Tulisharuhusiwa kuwasiliana na Bakari kujua mahitaji yake. Hivyo kama tutafikia makubaliano mazuri basi wewe “Priva” utakuwa mmoja kati ya watu wa kwanza kujua hilo” Injinia Hersi Said.