Wakati siku tano zijazo Young Africans itakuwa mjini Tunis, Tunisia kuikabiri Club Africain katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika, timu hiyo imepewa mbinu za kuifunga miamba hiyo.

Young Africans inahitaji ushindi au sare ya mabao itakaporudiana na Club Africain, Jumatano (Novemba 9), ili kutinga hatua ya makundi kwenye mashindano hayo baada ya juzi kulazimishwa suluhu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, timu hiyo imeambiwa kama ikitulia ina uwezo wa kuwashangaza Watunisia hao ambao wanatajwa kuwa na fujo na fitina za soka wakicheza nyumbani, ingawa pia inatajwa kupata upinzani kwa baadhi ya mashabiki ikiwa kwao.

“Kama Young Africans itajipanga vizuri itaifunga, waache kuzifikiria fitina na fujo za wapinzani, wao wapambane uwanjani kutafuta matokeo tu,” amesema nyota wa Kipanga, Abdillah Suleiman Kombo ‘Mido Kubwa’ aliyekuwa miongoni mwa wachezaji waliofungwa na timu hiyo nchini Tunisia.

Amesema ukiachana na matokeo ya karibuni ya kimataifa, timu hiyo si tishio sana kwenye ligi yao, huku akifichua kwamba Young Africans inachotakiwa ni kuidhibiti dakika 30 za kipindi cha kwanza na ikiweza itangulie kufunga lakini wakianza kufungwa basi timu hiyo itacheza hadi na waokota mipira.

“Wakiwa wanaongoza, hata waokota mipira wanajichelewesha kuwapa mipira, pia mashabiki wao wana fujo hadi za kurusha chupa uwanjani, lakini Young Africans wala wasizingatie, ingawa kwenye usalama askari wao wako vizuri.

“Vyumba vya kubadilishia nguo pia hakuna shida na hata hotelini, kuna ulinzi, sisi tulipokwenda askari wao walikuwa wengi na walitulinda kuhakikisha hatupati tatizo kuanzia hotelini hadi tunaingia uwanjani,” amesema Mido Kubwa.

Akiwazungumzia ndani ya uwanja, kiungo huyo alisema wana uwezo wa kuuchezea mpira na ukiwa kwa wapinzani wanahakikisha wanakukabia golini kwenu hawakupi nafasi.

“Hiyo ndiyo faida yao, hawapendi wapinzani wacheze wakiwa kwao na wana uwezo wa kufunga kwa kaunta sana, kama Young Africans ikijiamini na kushambulia kwa kushitukiza itapata matokeo.”

“Sisi walitufunga kwa mabao mengi ya ‘kaunta’, ingawa pia mabao yao wanayafunga kwa kutokea pembeni, wana kasi kubwa hasa dakika 30 za kwanza, baada ya hapo wanaanza kupunguza na kuchoka, Young africans ikiwafunga ndani ya muda huo watawavuruga,” amesema

Naye Kocha wa Kipanga FC, Hassan Kitimbe amesema endapo Young Africans itawamudu na kuwabana kipindi cha kwanza na kufunga bao la mapema, nafasi ya kusonga ipo.

Marubani kuanza mgomo shinikizo la madai
Papa Francis akutana na Sheikh Ahmed al-Tayeb