Msemaji wa Young Africans Haji Manara amesema Klabu hiyo imeweka mkazo wa kuzikataa ofa mbili zilizotua klabuni kwao, zikihitaji huduma ya kiungo kutoka Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Manara ametoa siri hiyo alipohiwa na kituo cha Wasafi FM mapema leo Jumatano (Juni 22), kwa kusema Young Africans haitamuuza Fei Toto kwa dau la chini ya Shilingi Bilioni Moja.
Amesema ofa zilizowafikia pasina kutaja klabu zilizotuma ofa hizo, haziendani na thamani ya kiungo huyo, ambaye mwishoni mwa mwezi Mei aliifungia Young Africans bao muhimu dhidi ya Simba SC, lililowapeleka Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
“Mchezaji kama Feisal sasa hivi ana mkataba, inakuja Klabu labda kutoka South Afrika inakuletea ofa ya USD 50,000 au USD 100,000 hatuwezi kukaa kuzungumza naye huyu mtu.
“Hapa katikati zimekuja ofa za baadhi ya timu, hatuwezi kumuuza Feisal Chini ya Tsh. Bilioni 1 sawa na Kama USD 500,000 hapo angalau tunaweza kuzungumza,” alisema Manara
Feisal Salum alisajiliwa Young Africans miaka mitano iliopita akitokea JKU ya visiwani Zanzibar, huku usajili wake ukihusika na klabu ya Singida Utd ambayo ilidaiwa kuwa ya kwanza kuinasa saini yake.
Makubaliano baina ya viongozi wa klabu hizo yalifanikisha safari ya Fei Toto kuondoka Singida Utd na kutua rasmi Jangwani.