Mkurugenzi wa Sheria klabu ya Young Africans Simon Patrick, amevunja ukimya kuhusu sakata la Kiungo kutoka Visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ ambaye ameendelea na msimamo wa kutaka kuvunjwa kwa mkataba wake na klabu hiyo.
Feisal ambaye tayari ameshashindwa kesi mbele ya Kamati Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ mara mbili mfululizo, aliwasilisha Barua ya kutaka kuvunjwa kwa mkataba wake na juzi Jumatano (April 12), shauri hilo lilisikilizwa kabla ya kuahirishwa hadi mwanzoni mwa mwezi Mei.
Akizungumza kupitia Yanga TV Mkurugenzi wa Sheria klabu ya Young Africans Simon Patrick amesema: “Hatumng’ang’anii Feisal lakini tunataka utaratibu ufuatwe. Kama tutaruhusu Feisal kuondoka kwa njia hii, kuna siku hatutakuwa na mpira maana mchezaji ataamka asubuhi na atasema hana furaha basi anaondoka”
“Huu ni uhuni ambao hautakiwi kuruhusiwa katika mpira. Ziko njia rasmi za kuvunja mkataba na zinafahamika hadi (FIFA)”
“Tunachotaka kanuni za mpira zisimamiwe, tusiruhusu MAHARAMIA wanaotumia fedha. Ikitokea wameruhusu hili nina hakika kabla msimu haujaisha atatokea mwenye fedha atawajaza Mamillioni atawaambia andikeni barua hamna furaha poteeni baadae mtaomba kuvunja mikataba mtaruhusiwa. Na hii sio kwa Yanga tu klabu zote”
“Sisi tunachokitaka sheria na taratibu zifuatwe, sisi hatuwezi kumruhusu aondoke kiholela japo sio kwamba tunamng’ang’ania. Akifuata Utaratibu TUTAMRUHUSU AONDOKE, Yanga ni kubwa kuliko mtu yeyote”