Uongozi wa Young Africans umetamba kulamba Bingo kwa kumsajili Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Kennedy Musonda wakati wa Dirisha Dogo la Usajili msimu huu 2022/23.
Musonda alisajiliwa Young Africans akitokea Power Dynamo ya nchini kwao Zambia, ambapo alifanikiwa kufunga zaidi ya mabao kumi katika Ligi ya nchini humo kabla ua kuwasili Tanzania.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema Uongozi wa juu wa klabu hiyo haukukurupuka kumsajili Musonda, kwani uliuyafanyia kazi kwa vitendo mapendekezo ya Benchi la Ufundi, ambayo yalipendekeza usajili wa mchezaji kama huyo.
Amesema uongozi ulitambua umemsajili mchezaji wa aina gani, na ndio maana haukusema lolote kwa kuwajibu baadhi ya wadau wa Soka la Bongo waliombeza Musonda siku chache baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza akiwa na Wananchi.
“Kila mchezaji anatimiza majukumu yake lakini Musonda huyu aliletwa maalumu kwa ajili michezo ya kimataifa hilo ni ya jambo ambalo linaonekana kwa sasa.
“Anafunga anatoa pasi za mabao unadhani nini tunakihitaji kutoka kwake bado kuna kazi kubwa ipo kwa kila mmoja mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,”
“Tulisikia kejeli za baadhi ya watu kuhusu Musonda, lakini tuliamua kukaa kimya kwa sababu tulijua kuna siku atawajibu kwa vitendo uwanjani. Na imekuwa hivyo.” amesema Kamwe.
Hadi sasa Musonda ameshaifungia Young Africans mabao mawili katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, akifanya hivyo dhidi ya TP Mazembe kisha US Monastir ambayo yamesaidia klabu yake kutinga Robo Fainali ya michuano hiyo.