Mshambulaiji kutoka DR Congo na Klabu ya Simba SC Jean Othos Baleke, amesema bado ana deni kubwa la kulilipa katika klabu hiyo ya Msimbazi katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baleke amekiri kuwa na deni hilo, baada ya kuwafurahisha Mashabiki wa Simba SC kwa kufunga mabao mawili, ambayo ni miongoni mwa mabao saba yaliyoizamisha Horoya AC ya Guinea, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika siku ya Jumamosi (Machi 18).

Baleke amesema anataka kuona akiendelea kuwapa furaha mashabiki wa Simba SC kwa kutoa mchango wa ushindi katika timu, ikiwemo kufunga na kutengeneza nafasi za mabao.

Amesema alisajiliwa Simba SC kwa ajili ya kufunga mabao pekee na sio kitu kingine, huku akishukuru ameanza vyema na timu hiyo, kwa kufunga mabao.

“Ninataka kuona nikitoa mchango katika kila mchezo nitakaoucheza katika timu yangu mpya ya Simba, kama sio kufunga basi nitengeneze nafasi kwa wenzangu.”

“Lengo ni kuwaona Mashabiki wetu wakiendelea kupata furaha ya ushindi, ninaamini nitafanikiwa katika hilo kutokana na ushirikiano mkubwa ambao ninaupata hapa Simba.”

“Kikubwa mashabiki waendelee kunipa sapoti ambayo wamekuwa wakinipa ili na mimi niendelee kufunga mabao,” amesema Baleke

Upande wa Ligi Kuu Tanzania Bara Baleke ameshaifungia Simba SC mabao matano, akiwa na Hat Trick aliyoipata kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.

US Monastir kumsajili Fiston Mayele
Young Africans: Tunamtaka yoyote Kombe la Shirikisho