Imefahamika kuwa Young Africans wapo katika mazungumzo ya kumsajili winga raia wa Ivory Coast, Aubin Kramo Kouame ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Asec Mimosas ya nchini humo.
Kramo mwenye umri wa miaka 27 anatumia zaidi mguu wa kushoto, huku akiwa anamudu vyema kucheza winga zote za kulia na kushoto ambapo msimu uliopita alifanikiwa kuifungia timu hiyo mabao tisa na kutoa pasi nane za mabao.
Chanzo kutoka nchini Ivory Coast kimeeleza kuwa Young Africans wapo mazungumzo ya kumsajili winga huyo ambaye ni moja kati ya wachezaji bora ndani ya Ligi ya Ivory Coast.
Pia chanzo hicho kimeongeza kuwa Young Africans wamehitaji pia huduma ya mchezaji mwingine kutoka timu hiyo anayekipiga katika nafasi ya beki wa kulia huku pia mazungumzo yakiwa yanaendelea kwa pande zote mbili.
“Ni kweli Young Africans wapo katika mazungumzo kwa ajili ya kumpata winga, Aubin Kramo ambaye amkuwa na misimu mizuri hapa Asec lakini sio huyo tu bali hata beki yule wa kulia, Kouassi Attohoula Yao pia Young Africans wanamhitaji na wapo pia kwenye mazungumzo.
“Hakuna jambo ambalo limekamilika mpaka sasa kutoka kwa wachezaji wote hao wawili ila Young Africans wapo katika mazungumzo nao ya kuwasjili kama wataafikiana na uongozi basi watasajiliwa,” kimesema chanzo hiko.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe akizungumza kuhusiana na usajili wa klabu hiyo amesema kuwa: “Young Africans kila msimu huwa inafanya usajili lakini usajili wa msimu ujao utakuwa usajili mzuri wenye manufaa kwa timu na sio kuwafurahisha watu.
“Hivyo wapenzi wa Young Africans watulie kwani uongozi unafahamu nini unafanya,” amesema kiongozi huyo.