Uongozi wa Kampuni ya Azam Media umesaini mkataba wa miaka 10 na klabu ya Young Africans wa uchakataji maudhui (Media Partnership), wenye thamani ya bilioni 34.8.
Mkataba huu unaifanya Azam TV kurusha matukio yote ya Young Africans kama michezo ya kirafiki, Mazoezi, Exclusive Interview za Viongozi na Wachezaji na matukio yote yanayoihusu klabu hiyo.
Mapema hii leo, pande hizo mbili zilitiliana saini katika hafla maalum iliyofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na waandishi wa habari.
Upande wa Azam Media uliwakilishwa na Tido Mhando ambaye ni Afisa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, huku Dkt. Mshindo Msolla akiiwakilisha Young Africans kama Mwenyekiti.
Sehemu ya makubaliano yaliopo kwenye mkataba uliosainiwa baina ya pande hizo mbili: Katika mwaka wa kwanza Young Africans watapokea kiasi cha Shilingi milioni 200 kwa kila mwezi, na mwaka unaofata kiasi hicho kitaongezeka kwa shilingi milion 20 kila mwezi mpaka miaka 10 itimie.
Endapo Young Africans watamaliza katika nafasi mbili za juu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara bila kutoka nje ya nafasi watapata Bonus ya Shilingi Bilioni 3 na itakuwa inaongezeka kila msimu.