Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umeanza mchakato mapema wa kutafuta mbadala wa Mawinga wa Kimataifa wa Klabu hiyo, Tuisila Kisinda na Bernard Morrison ambao tayari wamewashiwa taa nyekundu za kuachana nao mara baada ya Msimu huu kumalizika.
Katika kuhakikisha wanapata kilicho Bora Young Africans, wamevutiwa zaidi na Winga wa kimataifa kutoka nchini Mali na klabu ya AS Real Bamako Cheickan Diakite, mwenye umri wa miaka 18 ambaye aliwasumbua sana kwenye mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika uliomalizika kwa sare ya 1-1.
Tayari Uongozi wa Young Africans umeanza Mazungumzo ya awali na kinda huyo ikiwemo kuulizia Mkataba wake na Real Bamako na zaidi unataka kujiridhisha kiwango chake atakapokuja kwa mchezo wa Mzunguuko wanne wa Kundi D, Kombe la Shirikisho utakaopigwa Jumatano (Machi 08).
“Alicheza vizuri ule mchezo wa kwao, tumeongea naye vizuri lakini ngoja waje hapa kuna vitu ambavyo tunataka kujiridhisha zaidi kabla ya kufanya uamuzi,”
“Hatutaki kufanya uamuzi wa haraka, lengo letu tupate watu muafaka zaidi wa eneo hilo, unajua eneo hili la mawinga nalo limetuangusha sana, tuliwarudisha Morrison (Bernard) na Kisinda (Twisila) lakini bado hawajatupa kile ambacho tulikilenga”
“Tunataka kuanza mapema hesabu hizi ili tufanye uamuzi wenye afya kwa timu yetu kwa msimu ujao na tunataka kutumia mechi kama hizi za Kimataifa kuchagua watu bora ambao watakuja kutuongezea thamani ya kikosi chetu.” amesema mmoja wa viongozi wa Young Africans
Young Africans imejizatiti kufanya hivyo mapema ili kuepusha Presha, baada ya dirisha la usajili kufunguliwa mwishoni mwa msimu huu 2022/23, kuelekea msimu ujao wa 2023/24.