Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wameukana mpango wa kumsajili Mshambuliaji wa zamani wa TP Mazembe Thomas Emanuel Ulimwengu.
Young Africans inatajwa kuwa kwenye harakati za kusajili wachezaji wawili watakaoongeza nguvu kwenye kikosi chao, wakati wa kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili, ambacho kitafikia kikomo Januari 16.
Ulimwengu amekuwa akitajwa kuwa kwenye mpango wa kutua Jangwani kwa zaidi ya majuma mawili sasa, lakini Uongozi wa Young Africans kupitia Idara ya Habari na Mawasilino imekanusha mpango huo.
Mkuu wa Idara hiyo Ally Kamwe amesema hawana mpango wowote wa kumsajili Mshambuliaji huyo kutoka Tanzania, na wamekuwa wakishangazwa na taarifa zinazowahusisha na Ulimwengu.
“Hatuna mpango wa kumsajili Ulimwengu, tunashangazwa kuona kwenye Mitandao ya kijamii tukihusishwa na mpango wa kumsajili huyo mchezaji, ukweli ni kwamba tuna mipango mingine tofauti.” amesema Kamwe
Ulimwengu ameripotiwa kuwa jijini Dar es salaam, baada ya kuachana na TP Mazembe ya DR Congo aliyoitumikia katika vipindi viwili tofauti.
Mara ya kwanza Ulimwengu aliitumikia Klabu hiyo ya mjini Lubumbashi kuanzia mwaka 2011 hadi 2016, akicheza michezo 122 na kufunga mabao 33.
Aliondoka Klabuni hapo mwaka 2017 baada ya kujiunga na Klabu ya AFC Eskilstuna na Sweden, na baadae kutimkia Sloboda Tuzla ya Bosnia na Herzegovina.
Mwaka 2018 alirejea Barani Afrika akisajiliwa na Al-Hilal ya Sudan, mwaka 2019 akajiunga na JS Saoura ya Algeria kabla yakurtejea TP Mazembe mwaka 2020.