Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Klabu ya Young Africans Dominic Albinus amethibitisha kuwa klabu hiyo imeachana rasmi na mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Mbeya City Kibu Denis.
Kibu Denis alichukua nafasi kubwa katika vyonbo vya habari na mitandao ya kijamii, siku moja baada ya kuonesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Taifa Stars dhidi ya Malawi.
Albinus amesema Young Africans imesitisha mpango wa kumsajili nyota huyo wa Mbeya City, baada ya klabu hiyo kumuongezea mkataba kiungo Mapinduzi Balama ambaye alikuwa majeruhi kwa msimu mzima.
“Tulipanga kumsajili Kibu Denis lakini kwa sasa tumeona hakuna haja ya kuendelea na mkakati wa kumleta Young Africans kwa ajili ya msimu ujao, “
“Hivi sasa tumeona ni bora tukaendelea na Mapinduzi Balama ambaye anaifahamu vilivyo Young Africans, ameshasaini mkataba mpya na msimu ujao ataanza kucheza baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.” Amesema Albinus.
Mbali na Young Africans, klabu za Simba SC na Azam FC zilitajwa kuwa kwenye windo la kuiwania saini ya Kibu Denis katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu 2020/21.
Tayari baadhi ya klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara zimeanza kufanya usajili kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi, uliopangwa kuanza mwezi Septemba 2021.