Baada ya kuibanjua Mbeya Kwanza FC mabao 2-0, Kikosi cha Young Africans leo Jumatano (Desemba Mosi) majira ya asubuhi, kimeondoka Jijini Mbeya na kurejea Dar es salaam.
Young Africans inarejea Jijini Dar es salaam, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wanane wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaowakutanisha na watani zao wa jadi Simba SC Desemba 11, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini humo.
Kuelekea mchezo huo, Young Africans watakua wakichagizwa na ushindi bao 1-0 walioupata dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii mwezi Septemba.
Hata hivyo matokeo ya mchezo huo wa Ngao ya Jamii yataongeza upinzani mkubwa kwenye mchezo wa Desemba 11, kwani Simba SC hawatakuwa tayari kufungwa mara mbili na watani zao, huku Young Africans wakihitaji kuendeleza ubabe.
Young Africans iliyocheza michezo saba ya Ligi Kuu hadi sasa, inaongoza Msimamo kwa kufikisha alama 19, ikifuatiwa na Simba SC iliyocheza michezo sita na kufikisha alama 14.
Simba SC leo Jumatano (Desemba Mosi) itacheza mchezo wa mzunguuko wasaba wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold FC, kisha itasafiri kuelekea Zambia kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows utakaochezwa Jumapili (Desemba 05).
Baada ya kurejea kutoka Zambia Simba SC itaanza kambi rasmi ya kujiwinda na mchezo dhidi ya Young Africans.