Beki wa zamani wa Young Africans Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ ameweka wazi kuwa ili timu hiyo isonge mbele katika Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, inatakiwa kuhakikisha inapata matokeo mazuri katika Uwanja wa nyumbani tofauti na ilivyokuwa walipocheza dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Young Africans ilitolewa na Al Hilal baada ya kutoka sare ya 1-1 nyumbani, kisha ikapoteza ugenini nchini Sudan kwa kufungwa 1-0, hivyo ilipoteza kwa jumla ya 2-1.

Baada ya kufeli Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Young Africans imeangukia hatua ya mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ambapo watacheza dhidi ya Club Africain ya Tunisia, mchezo wa nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya Makundi kwenye Michuano hiyo.

Malima amesema: “Young African kama wanahitaji matokeo mazuri, wanapaswa kushinda hapa nyumbani kwa idadi nzuri ya mabao na wasiruhusu kufungwa, naamini wakifanya hivyo kazi itakua rahisi watakapocheza ugenini Tunisia.”

“Najua hata wale waraabu wanafahamu hilo, kwa hiyo watacheza kwa kujihami zaidi, lakini Young Africans inatakiwa kutumia nafasi ya kucheza nyumbani na kupata matokeo, naamini safu yao ya ushambuliaji ina uwezo mkubwa sana wa kupata matokeo katika mchezo wa keshokutwa Jumatano.”

“Unajua hii michuano ya Kimataifa haina njia ya mkato zaidi ya kuhakikisha unaitumia vizuri nafasi ya kucheza nyumbani kwako, hasa katika hatua kama hii ya mtoano, kama Young Africans watarudia makosa walioyafanya kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal, naamini yaleyale yatatokea tena watakapokwenda ugenini.”

“Cha muhimu hapa ni kuwa kitu kimoja kuanzia kwa Viongozi, Wachezaji na Mashabiki, ili kufanikisha mpango wa kuhisnda nyumbani, ninaamini Club Africain inafungika kabisa.”

Young Africans itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa keshokutwa Jumatano (Novemba 02), kisha itakwenda mjini Tunis-Tunisia kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa pili, ambao utaamua nani ataingia hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu wa 2022/23.

Kenyatta ahofia usalama, Rais amuagiza Waziri
Idadi waliokufa sherehe za Diwali yafikia watu 132