Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umesema hautaidharau kamwe klabu ya AS Ali Sabieh Telecom ‘ASAS’ ya Djibouti ambayo imepangwa nayo mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili yasije kuwakuta kama yaliyowakuta watani zao Simba SC walipotolewa pasipo kutarajia na klabu ya UD Songo 2019, na Jwaneng Galaxy, 2021.
Afisa habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kuwa hawatofanya kosa lolote la kuwadharau wapinzani hao kwa sababu kuna wakati Ligi ya Mabingwa Afrika kuwa na matokeo ya kushangaza.
Aliwatahadharisha baadhi ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo ambao akili yao inawaaminisha kuwa ASAS ni timu ndogo na kuiwaza zaidi El Merreikh ya Sudan ambao wanaweza wakacheza nao kama Wasudan hao watawatoa AS Otoho ya Congo Brazzaville.
“Ili kufikia malengo yetu ya mwanzo ya hatua ya makundi msimu huu ni lazima kwanza tushinde mechi yetu ya hatua ya awali dhidi ya ASAS, mechi ya kwanza Djibouti, ya pili hapa Dar es salaam na hapa wanachama na mashabiki wa Young Africans wanatakiwa wanielewe vizuri kabisa, nimeona mijadala ikianza eti tunarudi Sudan kucheza na El Merrikh sijui nini, hii tunakosea sana kwa sababu hata hao Wasudan wana mchezo dhidi ya Otoho, sasa ikitokea sisi akili yetu yote ikiwa inamuwaza Msudan akienda kutolewa na Wakongo Brazaville matokeo yake tunakutana na mpinzani ambaye hatukujiandaa naye,” amesema Kamwe.
Aidha amesema kama akili yao ikiiwaza sana El Merreikh mechi ya raundi ya kwanza, basi watapunguza umakini kwenye mechi ya hatua ya awali na kuweza kutolewa mapema kabla ya kufika huko walikoweka malengo yao.
“Tujifunze kwa watani zetu, mwaka 2019 na 2021 walitolewa na timu ambazo hawakutarajia, walitoka kufika hatua ya makundi lakini miaka hiyo wakaondolewa hatua ya kwanza kabisa, sisi hatutaki kupitia hayo,” amesema Kamwe na kuongeza,
“Hii ni michuano ambayo kuna wakati ina matokeo ya kushangaza, lazima tuchukue tahadhari katika kila mchezo na hatua tunayopita,” amesema.
Young Africans itaanzia ugenini nchini Djibouti kati ya Agosti 18-20 dhidi ya timu hiyo kabla ya kuja kurudiana nayo jijini Dar es salaam kati ya Agosti 25-27.
Kama itafanikiwa kuwatupa nje Wadjibouti hao itakutana na mshindi wa mchezo kati ya AS Otoho na El Marreikh kuwania kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Uongozi wa Young Africans umeweka wazi malengo yao ya kwanza ni kuhakikisha wanatínga hatua hiyo ya makundi.