Uongozi wa Yanga umechimba mkwara mzito kuwa hawatauchukulia poa mehezo wa mwisho wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya TP Mazembe kwani bado hawajamaliza hesabu zao.
Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuondoka Tanzania Machi 30, mwaka huu kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kukamilisha ratiba ya hatua ya makundi watakapovaana na TP Mazembe, Aprili 2, mwaka huu mjini Lubumbashi.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe, amesema: “Sehemu ya kikosi chetu ambacho hakıjaitwa kwenye timu za taifa kinaendelea na maandalizi ya mchezo dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa Aprili 2, DR Congo.
“Wengi tutauchukulia kwa wepesi mchezo huu kwa kuwa tayari tumeshafuzu hatua ya Robo fainali, lakini niwaweke wazi kuwa bado hatujafunga hesabu zetu, tunataka kuandika rekodi ya kumaliza msimamo tukiwa vinara, hivyo ni lazima tuhakikishe tunashinda mehezo huu.”
Young Africans tayari imeshakata tiketi ya kucheza Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku ikiongoza msimamo wa Kundi D baada ya kufanikiwa kukusanya alama 10 wakishuka dimbani mara tano.