Klabu ya Young Africans imetupwa nje ya Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) inayoendelea jijini Dar es salaam.
Young Africans imetupwa nje ya Michuano hiyo kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Express ya Uganda, katika mchezo wa mwisho hatua ya kundi A, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Wawakilishi hao wa Tanzania wanaondoka kwenye Kombe la Kagame wakiwa na alama mbili zilizotokana na matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi na kisha sare ya 0-0 dhidi ya Atlabara ya Sudan kusini.
Kupoteza mchezo wa leo Jumamosi (Agosti 07), kunaifanya Young Africans kuungana na Atlabara iliofungwa na Big Bullets mabao 2-0, kuyaaga mashindano hayo.
Big Bullets na Express zinatinga hatua ya nusu fainali zikiungana na Azam FC inayotokea kundi B, huku mshiriki mwingine wa hatua hiyo akitarajiwa kupatikana baada ya mchezo kati ya KCCA ya Uganda dhidi ya Messager Ngozi ya Burundi.