Imefahamika kuwa kikosi cha Young Africans kitacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Mabingwa wa Burundi Aigle Noir, katika Tamasha la Siku ya Mwananchi, ambalo litafanyika katika kilele cha Wiki ya Mwananchi.
Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki utachezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam, Agosti 30 sambamba na wachezaji wote wa klabu hiyo kutambulishwa kwa mashabiki na wanachama watakaojitokeza uwanjani hapo.
Tayari Young Africans imesajili wachezaji wanane wakigeni na mshambuliaji kutoka nchini Angola anatarajiwa kuwasili Dar es salaam kesho Jumanne.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Mwenyekiti wa Young Africans, Mshindo Mbette Msolla amesema washawasiliana na klabu hiyo na wamethibitisha watakuja.
Mwishoni mwa juma lililopita watani zao Simba SC walicheza dhidi ya Vital’O iliyomaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Burundi, na sasa Young Africans imerudi tena nchini humo kuwaleta mabingwa.
Msolla amesema mchezo huo wa kirafiki utategemea na ratiba watakayopewa na Azam TV baada ya mazungumzo, kufuatia siku hiyo ya Agosti 30 kuwa na mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba SC dhidi ya Namungo FC mjini Arusha.