Wakati Young Africans ikitarajia kusafiri kesho Jumamosi (Oktoba 15) asubuhi kuelekea Khartoum-Sudan tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Hilal, Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu hiyo imetoa kauli kuhusu maoni yanayoendelea kutolewa kupitia Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii.

Asilimia kubwa ya maoni yanayotolewa na Wadau wa Soka yamedhihirisha kuinyima ushindi Young Africans kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili, kufuatia matokeo ya sare ya 1-1, ilioyapata katika Uwanja wake wa Nyumbani mwishoni mwa juma lililopita.

Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema wanaheshimu maoni ya Wachambuzi na Wadau wote, ambao wamekua wakisema timu yao haiwezi kutinga Hatua ya Makundi ya Klabu Bingwa, watakuwa upande wao watakapofanikiwa kufika katika hatua hiyo.

“Kila Mchambuzi ambaye anafanya kazi kwenye Chombo cha Habari ambacho anafanya kazi anaaminika, hayupo kwa bahati mbaya. Young Africans hatuwezi kuingilia maoni yake, maoni yanatolewa sehemu yoyote duniani”

“Kama wanaamini Young Africans hawezi kufanya vizuri Khartoum, tunaheshimu maoni yao, sisi tunaamini kwenye mchezo wa mpira wa miguu. Hatuwezi kujibizana nao, kazi yetu ni kucheza mpira”

“Wanaosema timu yetu haiwezi kufuzu, tukifuzu watakuwa upande wetu na wataelezea kitaalam kwa nini tumefuzu. Kwa hiyo tunaheshimu mawazo yao na tunaomba waendelee kuizungumza timu yetu ili tupate mahali pa kuboresha kutoka kwenye maoni wanayotoa”

“Hatupo hapa kumzuia Mwandishi/Mchambuzi yeyote kuizungumzia Young Africans, tupo hapa kushirikiana na Vyombo vya Habari na Wachambuzi kuhakikisha klabu yetu inakuwa Brand kubwa Afrika” amesema Ally Kamwe

Young Africans inatakiwa kupata ushindi wa aina yoyote ama sare ya 2-2 na kuendelea ili kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.

Fiston Mayele: Tutaishangaza Afrika Jumapili
Jemedari Said: Simba SC ipewe heshima yake kimataifa