Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge, amefungua zahanati ya kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda katika Halmashauri ya wilaya Mbinga iliyojengwa kutokana na michango ya wananchi,Serikali na wadau wengine wa maendeleo.
Balozi Ibuge, amewapongeza wananchi hao kwa kuamua kutatua kero zao wenyewe bila kusubiri msaada wa serikali kwa kuchangia Sh. milioni 16 jambo linalopaswa kuigwa na wananchi wa maeneo mengine.
Mkuu wa mkoa amesema, zahanati hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi na kuwataka kuhakikisha wanaitunza na kulinda mindombinu ili ilete manufaa na kusisitiza kuwa,Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli zote za maendeleo.
Aidha Ibuge, amefurahishwa na kazi nzuri za maendeleo zinazofanywa na wananchi wa wilaya ya Mbinga na kuhaidi kuwa,serikali ya mkoa itaendelea kushirikiana na wananchi walioonyesha jitihada za kumaliza changamoto zao.
Amewataka,viongozi kuanzia ngazi ya vijiji,kata,na Wabunge kujitolea na kushiriki kazi mbalimbali za maendeleo zinazolenga kumaliza changamoto na kero zinazowakabili wananchi.
Naye Diwani wa kata ya Ruanda Deogras Mwingira alisema,wananchi wa kijiji hicho waliokuwa wanakabiliwa na kero ya upatikanaji wa huduma za afya kwa kipindi kirefu,sasa wameondokana na changamoto hiyo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo iliyoanza kujengwa tangu mwaka 2013.
Ameishukuru serikali na wadau waliofanikisha ujenzi huo,kuunga mkono juhudi za wananchi katika kusaidia na kuboresha sekta ya afya kwa wananchi ambao walikaa kwa muda mrefu kusubiri huduma za matibabu.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ruanda Idrisa Machumu alisema,ujenzi wa zahanati hiyo umefanyika kwa awamu tofauti na mpaka kukamilika jumla ya Sh.milioni 91,875,000.00 zimetumika.
Machumu alisema,Halmashauri ya wilaya kupitia mapato yake ya ndani imetoa Sh milioni 25,Serikali kuu imetoa Sh.milioni 50 na wananchi wamechangia Sh.milioni 16,875,000.00 ambapo zaidi ya wakazi 5,700 watanufaika.