Mkurugenzi wa Halmashauri Mji wa Geita, Zahra Michuzi amesema kichapo cha Simba SC cha mabao 5-0 wamekipokea kama funzo, ambalo litaendelea kuwakomaza katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba SC ilichomoza na ushindi huo ugenini Uwanja wa CCM Kirumba jana Jumapili (Desemba 18), mabao yakifungwa na John Bocco, Clatous Chotta Chama, Kibu Denis na Pape Ousman Sakho aliyefunga mawili.
Zahra ambaye ni mdau mkubwa wa Michezo na amekua bega kwa bega na Timu ya Geita Gold FC, ametumia ukurasa wake wa Instagram kuipongeza Simba SC, akikiri wazi kuwa kikosi chao kilionesha udhaifu na kujikuta kikiambulia adhabu ya kufungwa5-0.
Zahra ameandika: Hongereni sana @simbasctanzania kwa ushindi wa leo dhidi ya timu yetu pendwa ya @geitagoldfc fahari ya @geita_town_council hakika mmetufunza jambo, na nakir wazi kuwa udhaifu wetu ndio umetugharimu siku ya leo, hivyo tumekubali makosa yetu tumeyachukua na kuyafanyia kazi ili next time yasiweze kujitokeza tena, Naamini katika udhaifu wa leo ndio uimara wa kesho, muda utaongea,
Nahitaji vijana underground wapambanaji Tz nzima kwa ajili ya kukiimarisha kikosi cha geita,najua mpo huko lakini hamjapata nafasi ya kuonesha uwezo na maajabu yenu.