Wizara ya Habari ya Serikali ya Zimabwe, imesema mlipuko wa ugonjwa wa surua umesababisha vifo vya watoto wasiopungua 157, huku zaidi ya maambukizi 2,000 yakiripotiwa kote nchini humo.
Waziri wa Habari wa Zimbabwe, Monica Mutsvangwa ameyasema hayo na kuongeza kuwa kesi hizo zimekuwa zikiongezeka kwa kasi katika taifa hilo la kusini mwa Afrika, tangu mamlaka ilipotangaza habari za maambukizi ya kwanza yaliyopatikana mapema mwezi huu, huku vifo vinavyoripotiwa vikitarajia kuongezeka maradufu katika muda wa chini ya wiki moja.
Waziri huyo aliyekuwa akiongea na Wanahabari baada ya mkutano wa kila wiki wa baraza la mawaziri amesema, “Hadi kufikia Agosti 15 idadi ya jumla ya watu kote nchini imepanda hadi kesi 2,056 na vifo 157.”
Amesema, Serikali itaongeza chanjo ya ugonjwa huo ili kuokoa vifo vya watoto nchini humo, huku ikiomba sheria maalum inayoiruhusu kupata pesa kutoka kwa mfuko wa kitaifa wa maafa na kukabiliana na dharura hiyo.
Aidha, Waziri Mutsvangwa ameongeza kuwa, Serikali ilipaswa kushirikiana na viongozi wa kimila na kidini, ili kupata uungwaji mkono wao katika kampeni ya chanjo, na kusema waathiriwa wengi waliopoteza maisha hawakuchanjwa.
Wizara ya afya hapo awali ililaumu kuzuka kwa mikusanyiko ya madhehebu ya makanisa, na kusema Virusi vya surua huwashambulia watu hasa watoto wenye matatizo na kuleta madhara ya upofu, uvimbe wa ubongo, kuhara na maambukizi makali ya mfumo wa hewa.
Amezitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na upele mwekundu unaoonekana kwanza kwenye uso na kuenea kwa mwili wote, na kwamba hali hiyo inaweza kuzuiliwa na upataji wa chanjo.
Mapema mwezi Aprili 2022, Shirika la Afya Duniani (WHO), lilisema Afrika inakabiliwa na mlipuko wa magonjwa yanayoweza kuzuilika kutokana na ucheleweshaji wa utoaji chanjo kwa watoto, huku idadi ya wagonjwa wa surua ikiongezeka kwa asilimia 400.