Klabu ya Zalan ya Sudan Kusini imewasilisha rasmi maombi ya mechi zao zote dhidi ya Mabingwa wa Tanzania Yanga zichezwe hapa nchini kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zilizothibitishwa na uongozi wa klabu hiyo ni kwamba wapinzani hao wamewasilisha maombi hayo kuwa mechi zao mbili za hatua ya awali za Ligi ya Mabingwa Afrika zichizwe hapa nchini kama ambavyo kalenda ya mashindano ya CAF inavyoonyesha.
Tayari Zalan wameshakubaliwa maombi yao hayo huku wakitaja sababu ya viwanja vyao kukosa ubora wa kutumnika katika mashindano ya CAF kuwa ndio sababu kubwa.
Zalan ilitakiwa kuanzia kucheza nyumbani kati ya Septemba 9-11 mchezo ambao sasa utapigwa hapa nchini kisha timu hizo kurudiana tena baada ya wiki moja hapohapo Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hiyo inakuwa mteremko zaidi kwa Yanga ambao hawatatumia gharama kubwa walizotakiwa kutumia kuisafirisha timu yao wakibakiwa na kazi moja tu kuwatupa nje ya masahindano Wasudan hao.
Endapo Yanga itafuzu hatua hiyo itakutana na mshindi kati ya St George ya Ethiopia watakaokutana na matajiri wa Sudan Al Hilal.