Shirikisho la soka barani Afrika CAF limeridhia kuipa uanachama wa kudumu Zanzibar kuanzia hii leo.
Ombi hilo limeridhiwa na mkutano mkuu wa CAF unaoendelea mjini Addis Ababa nchini Athiopia.
“Ombi la Zanzibar limepita bila kuwekewa pingamizi, Zanzibar sasa ni mwanachama wa 55 wa CAF.” Uliandika ukurasa wa Twitter wa shirikisho hilo.
Kwa kupata nafasi hiyo, Zanzibar itakua na fursa ya kushiriki michuano yote inayoandaliwa na CAF, kama vile mataifa ya Afrika (AFCON), fainali za wanawake (AWCON) na fainali za vijana (AFCON U17 na AFCON 20).
Pia itakua na uhalali wa kuhudhuria mikutano mbalimbali pamoja na kupokea na kusimamia kozi mbalimbali na kupata fursa ya kupiga kura katika masuala muhimu ya CAF.
Kabla ya maamuzi ya mkutano mkuu wa CAF wa leo, Zanzibar ilikua inapata fursa ya klabu zake kushiriki michuano ya klabu bingwa barani Afrika na kombe la shirikisho.