Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar iko salama na mazingira ya kisiasa yanatoa fursa ya kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo kutokana na uwepo wa Serikali ya umoja wa kitaifa.
Mwinyi ameyasema hayo Ikulu ya Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Prof. Palamagamba Kabudi.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetoa kipaumbele katika kuimarisha Uchumi wa Bahari kuu hasa Uchumi wa bluu kama chanzo mbadala cha mapato kitakachosaidia kukuza uchumi na kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi.
Aidha, Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje umekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Serikali zote mbili kulinda mipaka yake ya bahari, kwaniulinzi huo pia utasaidia kuzuia na kupambana na uingizwaji wa dawa za kulevya nchini.
Kwa upande wake Prof. Kabudi ameupongeza uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kwa hatua ulizozichukua katika kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu visiwani humo na kwamba uwepo wa amani na utulivu utachangia kuleta maendeleo haraka kwa wananchi wa Zanzibar.