Ziara ya kimafunzo ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez sambamba na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mulamu Nghambi katika Klabu ya Al Ahly ya Misri, imezaa matunda baada ya klabu hizo mbili kukubaliana mambo kadhaa ya kimaendeleo.
Viongozi hao wa Simba waliondoka nchini mapema wiki hii kuelekea Misri kwa ajili ya kufanya ziara ya kujenga ushirikiano kwa klabu hizo mbili, ikiwa na malengo ya kupata uzoefu juu ya uendeshaji wa soka kisasa.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo wa Simba ulikutana na Rais wa Klabu ya Al Ahly, Mahmoud El Khatib, na kukubaliana mambo kadhaa ya kimaendeleo ambayo yataifaidisha nchi kisoka na Klabu ya Simba.
Katika ziara hiyo, uongozi wa Simba umesema moja kati ya mambo waliyokubaliana ni mpango wa kucheza mchezo wa kirafiki na Klabu ya Al Ahly ya nchini Misri kwa siku za hivi karibuni, ili kuongeza uhusiano mzuri zaidi kwenye masuala ya michezo.
Aidha, pia umesema wamekubaliana kushirikiana kwenye maeneo ya biashara, ufundi na uendelezaji wa wachezaji kwa kujenga kituo cha kukuza vipaji kwa ushirikiano na timu ya Al Ahly ikiwa ni kituo cha kwanza nje ya Misri (barani Afrika) ambacho kitaendeshwa na Simba na klabu hiyo.
Akizungumzia ziara hiyo, El Khatib amesema lengo kubwa la viongozi wa Simba ni kutaka ushikiriano na kujifunza mambo mbalimbali na kupata uzoefu wa kuendesha klabu hiyo katika mfumo wa kisasa.
“Tunaikaribisha Simba katika ushirikiano wetu, hasa kwa wajumbe hao kuja kujifunza na kupata faida katika uzoefu wa kuendesha klabu yao kuanzia katika uwanja wa michezo, biashara pamoja na mambo ya habari jinsi ambavyo tunafanya hapa kwetu,” amesema El Khatib.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez sambamba na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mulamu Nghambi wanaendelea na ziara yao nchini Misri, kwa kuitembelea klabu ya Zamalek ambayo ina historia ya ina yake barani Afrika.