Kocha wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane ametajwa kuwa chaguo bora zaidi la kuinoa klabu ya Chelsea na kuchukua nafasi ya Maurizio Sarri.
Mchezaji mwenzake nguli aliyewahi kung’ara na Klabu ya Arsenal, Robert Pires amemtaja akimpa sifa kuwa ndiye ‘shujaa atakayeineemesha Chelsea’.
“Nadhani Zidane anaweza kuwa chaguo bora zaidi kwa Chelsea. Anaweza kupata heshima kutoka kwa wachezaji wa Chelsea na kudhibiti nidhamu kwenye chumba cha kubadilishia nguo kama matokeo ya kazi nzuri aliyoifanya uwanjani na kama kocha,” Pires aliwaambia waandishi wa habari.
“Alikuwa mshindi na mpiganaji. Ana mafanikio mazuri kwenye Ligi ya Mabingwa kitu ambacho kinamvutia mmiliki wa Chelsea. Itakuwa habari njema sana kwa Ligi Kuu kama Zidane ataenda Uingereza,” aliongeza.
Hata hivyo, Pires ameushushia lawama uongozi wa Klabu ya Chelsea kwa namna wanavyoishi na mameneja wa klabu hiyo, akimuelezea Sarri kuwa ni kiongozi mzuri na mwenye historia nzuri ya mafanikio lakini wameshindwa kumtunza vyema.
Katika hatua nyingine, Pires alidai kuwa anamuona Kylian Mbappe kama mshindi wa Ballon d’Or katika siku za usoni.
“Ni nyota mkubwa na mchezaji mzuri sana, anaweza kufikia viwango vya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Ni muda tu ukifika atashinda Ballon d’Or,” alisema.
Alisema Mbappe anafanya vizuri katika Ligi ya aina yoyote na ameanza kupewa heshima kubwa uwanjani akiwa na umri wa miaka 20 tu.