Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Thiery Hitimana ametoa sababu za kukosekana kwa wachezaji Bernard Morrison na Pape Osmane Sakho katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Cambiaso Sports uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita (Jumamosi, Novembe 12).
Mchezo huo uliounguruma Uwanja wa Boko Veterans Jijini Dar es salaam, ulimalizika kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kuambulia sare ya 2-2.
Kocha Hitimana amesema kulikuwa na sababu za msingi kukosekana kwa wachezaji hao wawili katika mchezo huo, ambao ulikua wa kwanza tangu kikosi kilipokua chini ya Kocha Mkuu Fanco Pablo Martin.
Amesema Kiungo Mshambuliaji Bernard Morrison amelazimika kurudi nchini kwao Ghana kwa ajili ya kushughulikia hati yake ya kusafiria, huku Sakho akiwa bado hajarudia katika hali yake ya kupambana, kufuatia majeraha aliioyapata kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC.
“Morrison ameenda kwao Ghana kwa lengo la kubadili hati yake ya kusafiria, huku Sakho akiwa bado hajapona vizuri kuanza Mikiki Mikiki uwanjani.” amesema Kocha Hitimana ambaye alikaimu nafasi ya Kocha Mkuu baada ya kuondoka kwa Kocha Didier Gomes mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Simba SC inajiandaa na mchezo wa mzunguuko wa sita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Ijumaa (Novemba 19) Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.