Scolastica Msewa – Pwani.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Pwani, limeendesha programu ya mafunzo ya kuzima moto na uokoaji kwa wanafunzi zaidi ya 1,000 wa Shule mbalimbali kata ya Kisarawe, wakiwemo Walimu na Viongozi mbalimbali yatakayowasaidia kujiokoa pindi majanga yanapojitokeza.
Akizungumza baada ya zoezi hilo katika viwanja vya shule ya msingi Chanzige, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi Jenifa Shirima amesema mafunzo hayo yanatokana na kuanzishwa kwa utaratibu wa kutembelea maeneo mbalimbali ili kuelimisha namna ya kujikinga na majanga ya moto.
Amesema, zoezi hilo si la Wanafunzi pekee bali litaendelea mpaka majumbani ili kuhakikisha elimu ya zima moto na uokoaji inamfikia kila mwananchi pamoja na taasisi mbalimbali za binafsi na serikali na kwamba watatumia kifaa cha awali (Portable Fire Extinguisher), ili kuwasaidia wananchi namna ya kujiokoa pindi majanga yanapoteka.
Hata hivyo Shirima amesema Jeshi la Zimamoto lipo tayari kutoa msaada kwa wananchi pindi wanapokumbwa na majanga na kuwataka kutoa taarifa kwa kupiga namba 114 na atapatiwa ushirikiano kwa haraka.