Chama cha ACT Wazalendo kupitia kwa Kiongozi wake Mkuu Zitto Zuberi Kabwe kimemuandikia Rais Samia Suluh Hassan barua ya mapendekezo ili kuzifanya chaguzi kuwa za ushindani, huru na zenye uwanja sawa kwa vyama vyote vinavyoshiriki.
Chama hicho kimependekeza Rais Samia aanzishe mchakato wa kuifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya shughuli zake kwa Uhuru, “Tunapendekeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi iwe na Watumishi wake wanaowajibika kwa Tume tena wasiwe ni makada wa chama kimoja cha siasa.
Chama hicho pia kimependekeza kuanzishwa kwa mchakato shirikishi wa kupitia upya Sheria ya Vyama vya Siasa ili kuondoa vifungu vyote vinavyojinaisha siasa na kubana uhuru wa vyama vya siasa kutekeleza majukumu yake ili Vyama vya Siasa virejeshewe haki yake ya kisheria ya kufanya mikutano yake bila bugudha.
Aidha, wameomba kupitia taasisi zinazomilikiwa na Vyama vya Siasa nchini kama vile Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Rais aanzishe majadiliano miongoni mwa vyama ili kujenga kuaminiana na kutatua migogoro kwa njia za amani pale inapotokea.
Chama hicho kimependekeza Rais Samia anasihi vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kulingana na viapo vyake, kutojiingiza katika itikadi za kisiasa, kutenda haki kwa wote na kuachia mara moja wanachama wao na wa vyama vingine vya siasa waliokamatwa na kuwekwa magerezani nyakati za chaguzi kwa makosa ya kubambikiza.