Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT=Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa amesikitishwa sana na matokeo ya uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) uliofanyika jana usiku bungeni mjini Dodoma kwa upande wa Chadema.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook Zitto ameandika kuwa kuchagua watu bila kuangalia uwezo, uzoefu na uhusika wao kulingana na sehemu wanapotakiwa kuwepo ni kuliangamiza taifa, hasa ukizingatia changamoto zilizopo katika nchi hizo Afrika Masahriki.
Amesema kuwa nchi kama Rwanda, Burundi na Uganda zimepeleka wawakilishi mashuhuri na wenye uzoefu mkubwa katika bunge hilo kulingana na umuhimu wa shughuli zinazofanywa na bunge hilo.
“Jana usiku nilikuwa na hasira sana, kufuatia matokeo ya uchaguzi wa wawakilishi wa Tanzania kwenye bunge la Afrika Mashariki (EALA) haiwezekani kuchagua wabunge ambao hawana uwezo wa kwenda kujenga hoja, huku tukitegemea kupambana na changamoto za muungano wa nchi hizi za Afrika Mashariki”ameandika Zitto katika ukurasa wake wa Facebook.