Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Chama hicho kimeshapendekeza jina la mwanachama atakayemrithi Maalim Seif Sharif Hamad umakamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Zitto ameeleza hayo wakati wa hitma ya kumuombea Hayati Maalim Seif katika viwanja vya mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.
Zitto amesema kwa sasa kilichobaki ni kusubiri uteuzi utakaofanywa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi kwa mujibu wa Katiba.
“Bahati nzuri, Maalim Seif alikuwa ni kiongozi, alijua kuna siku Mungu atamchukua kwa sababu sisi sote lazima turejee kwa Mungu kama tulivyoambiwa katika mafunzo ya dini,” amesema Zitto.
“Kwa hiyo aliacha maelekezo ya nini kitokee iwapo atatangulia mbele ya haki. Namshukuru Mungu kwamba viongozi wa Chama wamefuata yale maelekezo yake kwa namna ambayo alituelekeza sasa umebaki wajibu wa Dkt Mwinyi kuyatekeleza hayo.”
Zitto amesema chama hicho kinaamini mwanachama aliyependekezwa ana uwezo wa kusimamia maridhiano na haki za Wazanzibari kama ambavyo Maalim Seif alivyokuwa akifanya.
Itakumbukwa Maalim Seif alifariki dunia Februari 17, 2021 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), tangu Februari 9, mwaka huu.