Kiungo kutoka nchini Morocco Hakim Ziyech anakaribia kukamilisha uhamisho wa kutoka Chelsea kwenda Klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia, huku mlinzi Kalidou Koulibaly pia akikaribia kuhamia huko Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa ESPN.
Chelsea inatazamia kuingiza fedha msimu huu wa majira ya joto, katika kukabiliana na madirisha mawili ya matumizi makubwa na kufadhili biashara zaidi mwaka huu, huku Ziyech na Koulibaly wakiwa miongoni mwa wachezaji kadhaa waliowaweka sokoni.
Mmiliki mwenza wa ‘Blues’ hao, Todd Boehly, hivi majuzi alikuwa nchini Saudi Arabia kwa mikutano na maofisa kadhaa wa soka, na kupatikana kwa wachezaji hao wa pembeni wa Chelsea ilikuwa miongoni mwa mada za mazungumzo.
Wakuu wa Saudi wamekubaliana na mpango huo haraka na vyanzo vimethibitisha kwamba Ziyech atakuwa mchezaji wa kwanza wa Chelsea kuelekea Mashariki ya Kati msimu huu wa majira ya joto.
Ziyech amekubali mkataba wa miaka mitatu kuungana na Cristiano Ronaldo katika Klabu ya Al-Nassr na hivi karibuni atafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kabla ya kuweka bayana kuhusu uhamisho huo.
Kwa Koulibaly, mazungumzo yanaendelea kuhusu kuhamia Al-Hilal.
Beki huyo wa kati wa zamani wa SSC Napoli amekataa uhamisho wa mkopo kwenda Serie A ili apate uhamisho wa kudumu kwenda Saudi Arabia.
Makubaliano kuhusu maslahi binafsi yanakaribia kukamilishwa, na mkataba wa miaka mitatu hadi 2026 pia uko mezani kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31.
Kipa Edouard Mendy pia amekubali kusaini mkataba wa miaka mitatu na Al Ahli, ambao sasa wanatafuta makubaliano juu ya ada ya uhamisho na Chelsea, Mkataba unatarajiwa kukamilika baadaye wiki hii.