Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic ameendelea kumuweka roho juu meneja wake Jose Mourinho, kufuatia kuibua hoja ya kutaka kuondoka Old Trafford mwishoni mwa msimu huu kwa masharti.
Taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti la Daily Mirror mapema hii leo zinaeleza kuwa, mshambuliaji huyo amegoma kusaini mkataba mpya hadi mwishoni mwa msimu huu, kwa lengo la kutaka kuona kama Man Utd itafanikiwa kucheza michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao.
Ibrahimovic ametangaza msimamo huo, kutokana na hitaji la kutaka kurejea kwenye michuano mikubwa barani ulaya ambayo hakuwahi kuikosa alipokua akizitumikia klabu za PSG, Inter Milan, AC Milan na FC Barcelona.
Hata hivyo, gazeti hilo halijaeleza ni wapi mshambuliaji huyo kutoka nchini Sweden atakapoelekea kama ataendelea na msimamo wake wa kutosaini mkataba mpya hadi mwishoni mwa msimu huu, ambapo mkataba wake wa sasa utakua unafikia kikomo.
Ibrahimovic alisaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Man Utd mwanzoni mwa msimu huu akiwa mchezaji huru, na mpaka sasa ameonyesha kusaidiana na wenzake ili kufikia lengo la kuipaisha Man Utd ili imalize katika nafasi nne za juu katika ligi ya England.
Majuma mawili yaliyopita Ibrahimovic alihusishwa na taarifa za kuwa mbioni kuelekea nchini Marekani kujiunga na Los Angles Galaxy, lakini wakala wake alipoulizwa kuhusu uvumi huo hakuzungumza lolote zaidi ya kuwataka waandishi wa habari kusubiri hadi mwishoni mwa msimu huu.
Tayari mshambuliaji huyo ameshaifungia Man Utd mabao 17 katika michezo 27 aliyocheza tangu mwanzoni mwa msimu huu.