Serikali nchini, imeiambia Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu kuwa zoezi la kuwahamisha wananchi waliojiandikisha kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga na maeneo mengine, ni kulinda haki za Binadamu.
Kauli hiyo, imetolewa Jijini Dodoma na baadhi ya Mawaziri wakati wa kikao kilichowakutanisha Mawaziri wa Tanzania na Timu ya Wataalamu kutoka Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu ikiongozwa na Kamishna wa Kamisheni hiyo, Dkt.Litha Ogana.
Hatua ya Timu ya Wataalamu ya Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu, kutua hapa nchini inakuja kufuatia malalamiko ya baadhi ya Asasi za Kiraia kuwa zoezi la kuwahamisha wananchi kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera, ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ameieleza Kamisheni hiyo kuwa zoezi la kuwahamisha wananchi limefuata haki za binadamu na lilikuwa shirikishi, na kusema bado wananchi wanaendelea kujiandikisha kwa hiari bila kushurutishwa kwa kuzingatia utu, heshima na haki za binadamu.