Kocha Mkuu wa Simba SC Zoran Maki amesema kusajiliwa kwa Beki wa Kati kutoka Ivory Coast Mohamed Ouattara katika kikosi chake, kumeongeza kitu cha ziada ambacho kitasaidia kwenye malengo ya klabu msimu ujao.
Ouattara alitambulishwa rasmi siku ya Ijumaa (Julai 22), baada ya kukamilisha taratibu za usajiliwa wake Simba SC, akitokea Al Hilal ya Sudan.
Kocha Zorana ambaye kwa sasa yupo kwenye Kambi ya Maandalizi ya msimu ujao mjini Ismailia-Misri, amesema kusajiliwa kwa Beki huyo ni faida kubwa kwa Simba SC, kutokana na uwezo wake wa kupambana.
Amesema mbali na Mchezaji huyo kucheza nafasi ya Beki wa Kati, pia ana uwezo wa kucheza nafasi ya Kiungo Mkabaji, lakini akasisitiza atamtumia kutokana na mahitaji ya timu.
Kuhusu ushindani katika nafasi ya Beki wa Kati, Kocha huyo kutoka nchini Serbia amesema, atatoa nafasi ya yoyote kuanza katika kikosi cha kwanza kutokana na uwezo na utayari utakaoonekana siku kadhaa kabla ya mchezo.
“Kuhusu Ouattara uwepo wa mchezaji wa daraja lake ndani ya kikosi chetu ni faida kubwa kwani ana uwezo mzuri wa kucheza Beki wa Kati na kutimiza majukumu ya kiulinzi,”
“Faida nyingine ya Ouattara ni kucheza kiungo mkabaji. Ana uwezo mkubwa na hilo kila mmoja atakuja kuliona kwenye michezo ya mashindano, ila kuhusu kucheza kikosi cha kwanza hilo sio rahisi kwani Onyango na Henock Inonga nao wapo kwenye ubora.”
“Ushindani kati yao watatu Ouattara, Inonga na Onyango wawili watakao kuwa bora zaidi katika maandalizi ya mchezo husika watapata nafasi.” amesema kocha Zoran Maki.
Ouattara amekua mchezaji wanne wa kimataifa kusajiliwa Simba SC katika kipindi hiki, akitanguliwa na Victor Akpan (Nigeria), Moses Phiri (Zambia) na Augustine Okrah (Ghana).
Wachezaji wazawa waliosajiliwa Simba SC ni Habib Kyombo kutoka Mbeya Kwanza FC na Nassoro Kapama kutoka Kagera Sugar FC.