Beki Mkongwe wa Geita Gold FC, Kelvin Yondani amesema anaisubiri kwa hamu michuano ya Kimataifa msimu ujao, baada ya klabu hiyo kufanikiwa kuwa sehemu ya klabu nne za Tanzania zitakazoshiriki michuano hiyo.

Geita Gold FC ilimaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu uliopita, na moja kwa moja ilijihakikishia kucheza Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Klabu nyingine zilizojihakikishia kushiriki Michuano ya Kimataifa ni Azam FC (Kombe la Shirikisho), Young Africans na Simba SC (Ligi ya Mabingwa Barani Afrika).

Beki huyo aliyejiunga na Geita Gold FC akitokea Polisi Tanzania msimu uliopita, amesema ana uzoefu na michuano hiyo na hana shaka katika ushiriki wake akiwa na klabu hiyo ambayo itashiriki kwa mara ya kwanza Kimataifa.

Amesema kwa uzoefu wake atahakikisha anatoa mchango mkubwa kwa kusaidiana na wenzake ili kuifikisha mbali Geita Gold FC, ambayo imepanga kuweka kambi nchini Burundi.

Katika hatua nyingine Yondani amesema, ana imani michuano hiyo ya Kimataifa itatoa fursa kwa wachezaji chipukizi kuviweka sokoni vipaji vyao, hivyo atahakikisha anahimiza kufanya hivyo kila watakaposhuka dimbani.

“Nimefurahi Geita Gold FC kuwa sehemu ya klabu zitakazowakilisha nchi kwenye Michuano ya Kimataifa msimu ujao, kwangu sina wasiwasi na hilo kwa sababu nina uzoefu mkubwa, nitahakikisha ninawasaidia wenzangu ili kufanikisha malengo yetu ya kufika mbali.”

“Hapa kuna wachezaji wengi chipukizi, wanapaswa kuitumia Michuano hii kama sehemu ya kujitangaza Barani Afrika na Duniani kwa ujumla, hawatapata nafasi nyingine kama hii, nitahakikisha ninawahimiza ili wapambane ili wafikie malengo ya kucheza nje ya nchi.”

“Young Africans imemsajili Stephane Aziz Ki alionekana akicheza dhidi ya Simba SC akiwa na ASEC Mimosas hata Luis Miquissone alitua Simba SC kupitia michuano ya CAF akiwa na UD Songo, hivyo ni fursa kwa wachezaji wenzangu wa Geita kujituma ili wajiuze kama wenzao,” amesema Yondani

Wapinzani wa Geita Gold FC, Young Africans, Azam FC na Simba SC kwenye Michuano ya Kimataifa msimu ujao 2022-23 watafahamika baada ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Waziri Ummy atoa ahadi kwa watumishi
Rais Samia awataka waendesha bodaboda, bajaji kuacha kutumika