Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewataka Wahitimu wa Mafunzo ya awali ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, kwenda kuzuia na kupambana na tatizo la rushwa kwenye miradi mikubwa ya kijamii inayoendelea kutekelezwa sehemu mbalimbali nchini kwani Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Simbachawene ameyasema hayo wakati wa hafla ya kufunga Mafunzo ya awali kwa Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi 370 wa TAKUKURU yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania mjini Moshi, Kilimanjaro na kuongeza kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora zaidi.
Amesema, mazingira hayo bora yatafanikiwa kwa kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ikiwemo elimu, afya pamoja na maji inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si kuingia katika mifuko ya watu wachache na kwamba wahitimu hao wakazuie na kupambana kwani rushwa ni ukosefu wa ustaarabu katika jamii.
“Kazi yenu kuu sio kupambana na rushwa bali kuzuia kabla haijatokea na ndio maana Serikali imeamua kuajiri watumishi wa taaluma mbalimbali wakiwemo Maafisa Ununuzi, Wahasibu, Wasanifu majengo na wataalamu wa TEHAMA ili mkawe mbele katika kuzuia kulingana na taaluma zenu na kushauri ipasavyo mnapoona kuna dalili za rushwa’’ amesisitiza Simbachawene.