Baada ya kukamilisha usajili wa kujiunga na Azam FC, Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Charles Zulu, ameahidi kupambana ili kumaliza kiu ya klabu hiyo kwa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao ndani ya kikosi hicho kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.
Zulu amesema anafurahi kufanya kazi na Azam FC, hivyo atahakikisha anashirikiana vema na wachezaji wenzake kufikia malengo ya timu hiyo.
Amesema hatawaangusha viongozi wa Azam FC na kocha wao, George Lwandamina, aliyependekeza kusajiliwa kwake katika kikosi cha timu hiyo kutokana na uwezo wake.
“Nafurahi kufanya kazi Azam FC, ni timu kubwa sana hapa nchini, hata Afrika Mashariki na Kati nina imani nikiwa hapa nitafanikisha malengo yangu ya kufunga na kutengeneza nafasi za mabao kwa wenzangu,” alisema Zulu.
Amesema atahakikisha anajituma na kujitoa ndani ya uwanja kuonyesha kiwango kizuri na kutowaangusha viongozi waliomsajili.”
Kikubwa ni ushirikiano mzuri nitakaoupata kutoka kwa wachezaji wenzangu ili kufikia malengo ambayo yanatarajiwa na kila mmoja wetu,” alisema kiungo huyo mshambuliaji kutoka Klabu ya Cape Town City ya Afrika Kusini.”
Zulu anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, mwishoni mwa juma lililopita alifanyiwa vipimo na kufuzu kisha kutia saini mkataba wa miaka miwili ndani ya viunga vya Azam Complex.
Azam FC imemalizana na kiungo huyo baada ya kufikia makubaliano na timu ya Cape Town City aliyokuwa akiitumikia akitokea Zanaco FC ya Zambia.