Polisi nchini Afrika Kusini, wanachunguza vifo vya watu 20 vilivyotokea ndani ya klabu ya usiku katika mji wa pwani wa London Mashariki, alfajiri ya Jumapili hii leo Juni 26, 2022.
Wengi wa waliofariki katika ukumbi wa klabu hiyo ya Enyobeni Tavern, wanadaiwa kuwa ni vijana wa umri kati ya miaka 18-20 ambao wanahisiwa kufariki kwa kukanyagana na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Taarifa za mitandao mbalimbali ya kijamii na vyombo vya Habari, zinaeleza kuwa vijana hao walihudhuria tafrija ya kusherehekea kumalizika kwa mitihani ya shule wakati wa majira ya msimu wa baridi.
Msemaji wa Idara ya Afya ya nchini Afrika ya Kusini Siyanda Manana amesema taarifa za awali zinaeleza kuwa miili ya Vijana hao ilikuwa imetapakaa kwenye meza na viti bila kuonesha dalili zozote za majeraha
“Kuna taarifa zinatoka kuwa miili mingi ilionekana chini bila ya kuwa na majeraha lakini kwa wakati huu hatuwezi kuthibitisha sababu ya vifo hivyo,” amefafanua Msemaji Manana.
Hata hivyo Manana amesisitiza kuwa Pilisi itafanya uchunguzi kwa kushirikiana na idara zingine ili kujua chanzo halisi na kusema Marehemu wamepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha serikali.
Awali, Waziri wa Polisi nchini Afrika ya Kusini, Bheki Cele alitarajiwa kuzuru eneo la tukio hii leo kujionea hali halisi, huku mmiliki wa klabu hiyo, Siyakhangela Ndevu, akisema aliitwa kwenye eneo la tukio hii leo majira ya asubuhi.
“Bado sijaelewa ni nini hasa kilitokea, lakini nilipopigiwa simu asubuhi niliambiwa mahali pale palikuwa pamejaa na baadhi ya watu walikuwa wakijaribu kuingia kwa nguvu ndani ya Tavern,” alisema.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi wa Eastern Cape Nomthetheleli Lilian Mene akiwa katika eneo la tukio alisema madai ya mkanyagano yamesimuliwa na watu wengi huku Brigedia Kinana akiwaambia waandishi wa habari kuwa miili mingi ilikutwa sakafuni ndani ya ukumbi huo.