Serikali, imewataka Wanawake wenye umri wa kuzaa au wanaopanga kupata watoto kula vyakula vyenye kuongeza madini ya ‘Folic’ itakayomkinga mtoto na changamoto za maradhi ikiwemo ya mgongo wazi na kichwa kikubwa.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameyasema hayo jijini Dar es Salaam mara baada ya kushiriki mbio za marathon zilizoandaliwa na Taasisi ya Mifupa (MOI), za kuchangisha fedha za matibabu kwa Watoto 200 wenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi.

“Tatizo la Watoto kuzaliwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi linatokana na ukosefu wa ‘Folic Acid’, sasa wanawake walio kwenye umri wa kuzaa na walio katika mipango ya kupata Watoto waanze kutumia vyakula ambavyo vitawapa madini hayo,” Amebainisha Waziri Ummy.

Amesema, tatizo la Watoto kuzaliwa na changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi bado lipo nchini, huku takwimu zikionyesha Tanzania ni nchi tatu kati ya tano za Bara la afrika zenye Watoto wengi wanaozaliwa na changamoto hiyo nyuma ya Algelia na Ethiopia.

Aidha, Ummy ameongeza kuwa kwa hapa nchini kila Watoto watatu katii ya 1000 wanaozaliwa wana tatizo la mgongo wazi na kichwa kikubwa, na kwamba takwimu za Watoto wanaozaliwa kila mwaka hufikia takribani milioni 2, na kufanya Watoto 6000 kila mwaka kuzaliwa na matatizo hayo.

“Lengo letu ni kuzuia watoto wenye matatizo haya wasizaliwe hapa nchini, kwa hiyo tutaendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za uzazi hususani kabla ya kujifungua, wakati wa ujauzito na kujifungua” amesisitiza Waziri huyo wa Afya.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha madini ya fluoric yanapatika kwa urahisi katika ngazi zote za kutolea huduma za afyahadi ngazi ya Zahanati, na kuwataka Wakunga na Wauguzi watoe rufaa watoto wenye matatizo hayo.

Kwa upande wa Wazazi na Walezi, Waziri Ummy amewataka kuwahi matibabu katika vituo vya afya na kuacha kuwaficha Watoto wanaozaliwa na tatizo hilo ili waweze kufanyiwa upasuaji na kupata uponyaji.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Taasisi ya Mifupa (MOI), Prof. Charles Mkony amemshukuru Waziri Ummy kwa kuendelea kuiunga mkono MOI kutoa huduma bora kwa Watanzania sambaba kushiriki mbio hizo.

“Taasisi ya MOI imekuwa ikitoa huduma za matibabu kwa Watoto wenye matatizo hayo na Watanzania, Mashirika na watu binafsi wenye uwezo wa kiuchumi wanatakiwa kuchangia katika matibabu ya Watoto hawa wasio na uwezo wa kujilipia,” amesema Prof. Mkony.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa (MOI), Dkt. Respicious Boniface amesema kupitia fedha walizoweza kuchangisha, wameweka kambi ya kuanza kutoa huduma za matibabu na kwamba tayari Watoto 20 wameshapatiwa matibabu.

Serikali yatangaza nafasi 736 za ajira mpya
G7 yakuna kichwa mfumuko wa bei Duniani