Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdehack Benchikha amebadili gia ya usajili kwenye timu hiyo na sasa amesema anata ka kupata wachezaji bora wazawa na wawili tu wa kigeni.
Simba SC ilikuwa inatarajiwa kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha hili dogo, lakini taarifa zinasema kuwa kocha mkuu wa timu hiyo anataka wachezaji wawili tu kutoka nje ya nchi.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikosi hicho kinasenma kuwa kocha huyo anataka wachezaji wawili kwenye dirisha hili dogo, mmoja mshambuliaji na kiungo mkabaji, lakini akiomba aongezewe nguvu kwa wachezaji wa ndani.
Benchikha raia Algeria mwenye misimamo mikali, amesema hataki kumuona mchezaji anayesajiliwa kwenye timu hiyo ambaye atakuwa hatumiki kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
“Kocha ameshatoa mapendekezo yake, lakini ni tofauti na wengi walivyokuwa wanafikiri kwani amesema apewe angalau wachezaji wawili wa kimataifa kwenye dirisha hili, lakini wawe ni wale ambao atawatumia kwenye Ligi ya Mabingwa, yaani hataki asajiliwe mchezaji ambaye hatatumika kwa msimu huu.
“Anasema tageti yake kubwa ni kufika kuanzia Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa na kuendelea, hivyo itakuwa haina maana kama atasajiliwa mchezaji ambaye tayari ametumika msimu huu,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, mchezaji akiwa ameshatumika kwenye michuano ya CAF msimu huu akihama hana nafasi ya kutumika kwenye timu nyingine kwa msimu huo.
“Kocha anaamini kuwa wachezaji wazuri wanaweza kupatikana, lakini siyo sawa na kipindi cha dirisha kubwa, hivyo anaamini maboresho makubwa ya kikosi yatafanyika kuanzia Julai mwakani.
“Hata hivyo, ametaka Simba SC ihakikishe wanafanya usajili mzuri wa ndani, huku ikionekana kuwa anaweka nguvu pia kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi linaloanza leo Alhamis,” kimesema chanzo hicho.
Tangu Benchikha ametua nchini, wachezaji wengi ambao walikuwa hawapati nafasi kwenye kikosi cha Simba SC wamefanikiwa kucheza huku kila mmoja akionyesha kiwango chake.
Timu hiyo kwa sasa ipo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoanza leo Alhamis (Desemba 28) Visiwani Zanzibar, huku ikiwa Kundi B pamoja na Singida FG ya Tanzania Bara, APR kutoka nchini Rwanda na JKU ya Zanzibar.