Katika hali isiyokuwa ya kawaida na isiyozoeleka au nadra kutokea, Oktoba 8, 2021 Rais wa mpito wa Guinea ambaye alitwaa madaraka baada ya kufanya mapinduzi, Kanali Mamady Doumbouya alitoa somo la kizalendo na la maisha kwa Taifa lake, Afrika na Dunia.
Ilikuwa ni siku ya ijumaa, ambapo alipanga kuhudhuria Ibada katika Msikiti wa Boulbineti uliopo jijini Conakry na kama ilivyo ada ya heshima kwa Viongozi wa kitaifa, Kanali Doumbouya aliandaliwa nafasi ya mbele Msikitini.
Lakini katika hali ya kustaajabisha, na kuwashangaza wengi alipofika na kukuta watu wamejaa Msikitini kiasi wengine wamekaa njee, kanali Doumbouya naye aliamua kubakia nje na Wananchi wa kawaida na kuketi chini.
Imamu alipata taarifa hiyo na kuwahimiza wazee ili wamshawishi kwenda kukaa katika nafasi yake aliyoandaliwa, lakini walipofika kumpa ujumbe jibu lake liliwastaajabusha.
Alisema, “Hakutakiwi kuwa na matabaka katika nyumba ya kumwabudu MUNGU, watu wote ni sawa wakiwa Msikitini.”
Sina shaka utakubaliana nami kwamba ukiwa na hofu ya MUNGU na ukaishi huku ukitambua kwamba huijui kesho yako, basi mambo yatakuwa rahisi kwani watu wengi walipongeza tukio hili lenye uthamani ya utambuzi wa maisha ya Mwanadamu.